Mbali na Nyumbani

Adam Shafi

Artwork by Shay Xie

Hamu ya Kusafiri Imenishika

Nilipokuwa nikisoma Chuo cha Ualimu cha Seyyid Khalifa, hapo Beit-el-Ras kuanzia mwaka 1957, kila ilipofika magharibi mimi nilikaa juu kwenye roshani kubwa iliyokuwepo mbele ya bweni langu. Nilikaa hapo nikiangalia baharini. Tokea utotoni mwangu mandhari ya bahari yalikuwa ni kitu kilichonifurahisha sana. Nyumbani, baba yangu alikuwa akinipiga kila siku kwa sababu ya mapenzi makubwa niliyokuwa nayo kwa bahari na mchezo wangu wa kila siku baharini. Si kama akinipiga kwa sababu hakupenda nicheze baharini lakini alikuwa na hofu, mwanawe mpenzi,nisije nikachukuliwa na "chunusi" nikafia baharini.

Kwa hivyo, mimi nilikuwa nikisimama hapo kwenye roshani, mbele ya bweni langu. Hapo nilikuwa nikiiangalia bahari na vyombo vilivyoingia na kutoka katika bandari ya Unguja. Hapo, ndiyo njia kubwa ya meli, merikebu na vyombo vyote vya baharini vinavyoingia Unguja kutokea kaskazini kuelekea kusini na kutoka kusini kuelekea kaskazini. Baina ya mwezi Desemba na Machi, wakati wa pepo za Musim, majahazi, mitepe na mabedeni huingia kwa wingi kutoka Arabuni, India, Ghuba ya Uajemi na Somalia na baina ya mwezi April na Juni vyombo hivyo hupita hapo hapo vikirudi vilikotoka.

Mimi nilikaa hapo kwenye roshani nikiviangalia vyombo hivyo jinsi vilivyokuwa vikitelezajuu ya uso wa bahari. Wakati huo huwa ni magharibi, jua likitua. Ukiangalia kule mbinguni ulikuwa unaziona mbingu jinsi zilivyokuwa zimekoza rangi ya mchanganyiko wa dhahabu na hudhurungi. Mara nyingine utayaona mawingu yametulia matulivu kama busati lililotandikwa na mara nyingine zimezonganazongana na kujipanga mafungu mafungu, rangi zimeingiliana, manjano, zambarau na hudhurungi. Saa hizo, jua huwa linawaka, jekundu kama mpira mkubwa wa moto likititia chini ya bahari utadhani likifukuzwa pale lilipokuwepo likikimbilia pengine. Siku nyingine nilikuwa nikisimama hapohapo kwenye roshani wakati wa usiku, pale mwezi ulipokuwa mkamilifu. Niliiangalia bahari ilivyometameta kama fedha chini ya mwanga mkali wa mbalamwezi na vyombo navyo vikiingia au vikitoka. Wanafunzi wenzangu, wengi wakijua kwamba wakati kama huo usingeliweza kunipata popote ila hapo kwenye roshani. Labda wakati mwingine nilikuwa nikienda ufukweni kabisa ili niwe karibu zaidi na bahari. Ilipotokea hivyo basi nilikwenda Kilosa Beach. Hilo lilikuwa ni jina la ufukwe uliokuwa karibu sana na chuo chetu, jina ambalo sisi wenyewe wanafunzi tuliupa ufukwe huo. Huko nilikwenda na nai yangu ambayo nilijua vizuri kuipiga.

Kwa muda wa miaka mitatu niliishi katika hali hiyo na hapo ndipo ibilisi wa safari alipoanza kuniingia kidogo kidogo na mimi nikatamani kuwa abiria katika vyombo vile nilivyoviona vikiingia na kutoka. Katika hilo nilipata mshabiki mwenzangu. Mohammed Masoud Seif.

Mohammed alikuwa akiwajua watu wengi walioondoka Unguja zamani kwa majahazi na mabedeni na walikwisha fanya maskani Dubai, Kuwait na hata Uingereza. Basi Mohammed Masoud alikuwa akinihadithia nani alikuwa wapi, alifika vipi, mipango ya safari yake ilikuwa vipi, na mimi nilikuwa nikimsikiliza kwa utulivu na hamu kubwa.

Mimi na Mohammed, sote tulikuwa maskauti katika kikosi cha kumi na nne cha pale chuoni petu. Yeye alikwisha kwenda Uingereza katika kambi ya "Jamboree" kwa hivyo na ya Uingereza pia akiyajua. Alikuwa heshi kunisimulia juu ya maisha mazuri wanayoishi watu wa Zanzibar huko Portsmouth na fursa nyingi za masomo zinazopatikana huko Uingereza.

Mimi akili yangu haikuwa katika starehe na maisha mazuri. Nilikuwa nikipenda kusoma na kila siku nilikuwa nikiwaza lini nitaingia katika chuo huko Ulaya. Basi mimi na Mohammed Masoud tulikaa na kupanga. Tutasafiri kwa jahazi mpaka Kuwait. Huko, tutafanya kazi kwa muda na tukishakusanya pesa za kutosha tutaendelea na safari yetu mpaka Uingereza. Mimi na Mohammed Masoud tukawa marafiki wakubwa, kila wakati tulikuwa pamoja. Kila mahali tulikuwa pamoja. Hatukuwa na mazungumzo mengine isipokuwa safari yetu ya pamoja kutoka Zanzibar hadi Kuwait na baadaye mpaka Uingereza.

Mohammed Masoud aliumwa ghafla. Alipata homa kali ya malaria, akafa. Mungu amrehemu, amlaze mahala pema peponi. Kifo chake kiliniathiri sana. Mimi na yeye tulijenga usuhuba mkubwa sana kiasi ambacho Mohammed alikuwa kama ndugu yangu. Tuliyokuwa tukiyazungumza na kuyapanga hatukuyazungumzakama ni mchezo wa kitoto bali tuliyapanga ili tuyatekeleze kwelikweli, kwa hali yoyote ile.

Nilisikitishwa sana na kifo cha Mohammed lakini nilijenga mori mpya na nia yangu ya kusafiri ilibakia palepale ila sasa mipango yote ilinibidi niiandae peke yangu. Niwatafute hao wanaowajua manahodha wa vyombo, niulize uwenyeji huko Kuwait au Dubai na la muhimu zaidi lilikuwa ni pesa kwa ajili ya hiyo safari yangu.

Nilimweleza baba yangu kwamba nilitaka kwenda Ulaya kusoma. Aliniuliza bei ya nauli kwa meli mpaka huko Ulaya.

Wakati huo ilikuwa nadhani shilingi elfu moja mia nane, kwa meli za Kifaransa, Ferdenand de Lesepes au Periloti, kutoka Unguja mpaka Marceiles. Kutoka hapo ningelivuka kupitia English Channel kwa bei ndogo tu mpaka Uingereza.

Nilipomtajia bei hiyo baba yangu, alinywea kama aliyemwagiwa maji ya baridi. Hata mimi mwenyewe nilimwonea huruma. Angelipenda sana kunipeleka mimi mwanawe wa kwanza kwenda kusoma Ulaya lakini uwezo huo hakuwa nao. Baba yangu akipenda sana watoto wake tusome. Yeye mwenyewe alikuwahakusoma. Hakuwahikuuonamlango wa skuli hata siku moja. Alijisomesha mwenyewe mpaka akajua kusoma gazeti na kuandika kidogo. Gazeti lake kubwa lilikuwa Afrika Kwetu lililokuwa likitolewa na marehemu Bwana Mtoro Rehani. Alikuwa bingwa wa kufanya hesabu za kujumlisha na kutoa na aliweza kujumlisha tarakimu hata kama zilikuwa zimejipanga msururu wa mita nzima.

Mimi na mdogo wangu Saad, kila tulipofanya uzembe wowote uliohusiana na masomo yetu skuli, alitugomba sana. Kil alipotugomba alikuwa hupiga kelele kwa hasira na kutwambia, "Mimi baba yenu ni mjinga kwa sababu sikusoma lakini sitaki nyinyi watoto wangu muwe wajinga kama mimi."

Maneno hayo kwake yalikuwa kama nyimbo ambayo kila wakati alituimbia. Ameiimba sana kiasi ambacho mpaka hii leo bado naisilda ikivuma masildoni mwangu.

Baada ya siku hiyo, sikumwambia tena baba yangu kuhusu nia yangu ya kwenda kusoma Ulaya. Nilijua kwamba alikuwa hana uwezo na kumchagiza anipe pesa kwa safari yangu hiyo ingelikuwa ni kumtia simanzi tu. Maisha yetu yalikuwa ya kimaskini lakini hayakuwa ya ldfukara. Nakumbuka nilipokuwa nikisoma Skuli ya Gulioni, wakati mwingine nilikuwa nilifukuzwa skuli kwa kushindwa kulipa ada ya shilingi thelathini tu kwa muhula wa miezi mitatu, seuze leo, namtajia elfu nzima na mia nane juu. Niliapa kwamba pesa za safari ningelizitafuta mimi mwenyewe, kwa nguvu zangu, kwa jasho langu.

Baada ya kufa Mohammed Masoud Seif, nilipata mshabiki mwingine wa safari yangu hiyo. Naye alikuwa na mori wa safari kama ule niliokuwa nao mimi. Alikuwa Khamis Mohammed Nura,[1] mwanafunzi mwenzangu hapo hapo Chuo cha Ualimu, Khamis hakuwa na shida ya pesa. Baba yake alikuwa nazo kidogo. Alikuwa na biashara ya kuendesha teksi na alikuwa mmoja wa waendesha teksi maarufu mjini Unguja. Kwa hivyo pesa mbili, tatu, hazikumpa shida. Khamisi alifanikiwa kumfanyia baba yake lµinimacho, akamdanganya, akazitia pesa mkononi, akaondoka kwa jahazi mpaka Kuwait akiniacha mimi na safari yangu ya hadithi.

Na mimi nilianza kuzitafuta pesa. Nilianzisha mradi wa dobi pale chuoni. Yeyote aliyetaka kufuliwa au kupigiwa pasi nguo zake mimi nilianza kutoa huduma hiyo kwa malipo. Hapo chuoni sabuni tukipewa bure, umeme ulikuwepo, pasi zilikuwepo, kilichotakiwa ni nguvu zangu na mimi nguvu nilikuwa nazo. Kwa hivyo mradi wangu ulishika kasi, nikapata wateja chungu nzima.

Jumamosi, wakati wanafunzi wenzangu wakienda kutembea majumbani kwao kuwatembelea wazazi wao au wakienda mjini kwa matembezi ya kawaida na kujiburudisha kwa kuangalia sinema, mhni nilikuwa kazini. Nilibakia hapo chuoni nikifua na kupiga pasi. Nikawa ndiye dobi wa chuoni hapo. Kwa kazi hiyo, nilipata pesa za kutosha na nilitengeneza pasi ya kusafiria. Siku niliyoipata pasi hiyo nilifurahi kupita kiasi nikaona sasa safari kweli ipo. Ilikuwa pasi ya Kiingereza iliyoniruhusu kwenda popote pale duniani.

Niliificha pasi yangu ya kusafiria, nikaienzi kama vile nilivyozienzi mboni za macho yangu. Waliojua juu ya mpango wa safari yangu walikuwa wachache tu. Kila siku zilivyokwenda ndivyo mori wa safari ulivyozidi kunipanda. Aliyezidi kuupandisha mori huo alikuwa Khamis Mohammed Nura. Yeye alikuwa akiniandikia barua, takriban kila mwezi. Tokea alipofika Kuwait kwa jahazi mpaka alipoondoka Kuwait. Aliniarifu juu ya kufika kwake London na kunieleza juu ya maisha ya huko Uingereza. Nilimuhusudu nikamwona kama aliyefika mwezini.

Wakati huo nilikuwa katika mwaka wangu wa tatu hapo Chuo cha Ualimu cha Seyyid Khalifa Teacher Training College. Nilikuwa mwaka wa tatu kwa sababu mwaka wa pili ilinibidi nirudie darasa kwa sababu ambazo mpaka hivi leo mimi nashindwa kuzielewa.

Inasemekana kwamba serikali ya Kiingereza ilikuwa ikitaka kupunguza idadi ya wanafunzi wapya wa kuingia katika chuo hicho. Kwa hivyo ilibidi ba.adhi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza warudie darasa ili waungane na wale wachache watakaochukuliwa. Pia baadhi ya wanafunzi wa mwaka wa pili warudie darasa ili waungane na wale wachache watakaomaliza mwaka wa kwanza. Mimi nikawa miongoni mwa wale wa mwaka wa pili waliotakiwa warudie darasa.

Ilikuwa tumemaliza muhula wa kwanza wa mwaka 1960. Chuo kilifungwa kwa mapumziko ya muhula huo. Kazi yangu ya udobi iliniiingizia pesa za kutosha. Wakati huo ambao chuo kilikuwa kimefungwa nilikuwa na ldasi cha shilingi mia saba kibindoni. Nilikwenda katika ofisi ya Karimjee Jevanjee iliyokuwepo karibu na Ngome Kongwe. Wao walikuwa na idara ya uwakala wa meli.

Pesa nilizokuwa nazo hazikutosha kwa nauli ya kutoka Zanzibar hadi Uingereza.

Kwa hivyo ilinibidi nikate tiketi ya safari ya kutoka Unguja mpaka Aden. Nilitegemea kwamba nitakapofika Aden ningelitafuta kibarua chochote kile ili niweze kupata pesa ambazo zingelinitosha kuendelea na safari yangu hadi Uingereza. Nilikata tiketi yangu hapo kwa wakala wa meli katika ofisi ya Karimjee. Wakati huo safari yangu ikawa imeiva. Haikuwa safari ya hadithi tena.

Nyumbani nilikuwa nikilala chumba kimoja na mdogo wangu Saad. Tulikuwa tukiishi nyumbani kwa bibi yetu Bibi Asha binti Kassim. Hakuna aliyejua kuhusu safari yangu hiyo hapo nyumbani. Waliojua kuhusu safari hiyo walikwa ni wachache tu. Ni baadhi ya marafiki ambao walinisaidia pesa kidogo kwa safari hiyo. Msaada mkubwa wa pesa kwa ajili ya safari yangu niliupata kutoka kwa Khamis Mohammed Nura ambaye wakati huo alikuwa tayariyuko London. Yeye aliniletea Pauni mia mbili za Kiingereza. Wengine ambao walinisaidia kwa kunichangia pesa na ambao bado nawakumbuka ni Mohammed Said Mohammed, Bilal Gharib na rafiki yangu mpenzi, Abdalla Mwinyi Khamis. Hawa nawashukuru sana.

Mwenye kuhitaji shukrani za pekee ni Abdalla Mwinyi. Urafiki wetu mimi na yeye umepindukia ile daraja ya urafiki wa kawaida na tumekuwa kama ndugu wa baba mmoja mama mmoja. Yeye alikuwa ndiye mwandalizi mkubwa wa safari yangu na ndiye niliyemwachia jukumu la kuwasaidia wadogo zangu baada ya mimi kuondoka. Alifanya hivyo.

Siku ya safari sikuwa na mizigo mingi. Nilikuwa na mfuko mdogo tu wa kuchukua mkononi na ndani ya mfuko huo mlikuwa na suruali mbili na mashati mawili. Siku hiyo niliamka asubuhi nikamuaga Saad na kumwambia kwamba nakwenda mandar Chwaka.

Ulikuwa mwezi wa Ramadhani na safari za mandar si za kawaida wakati wa mwezi huo. Saad alikuwa usingizini kwa hivyo hakutaka kujua zaidi kuhusu safari yangu hiyo ya mandar. Nilikwenda zangu mpaka kwa Abdalla Mwinyi. Alinipakia kwenye skuta yake na kunipeleka bandarini.Naondoka Zanzibar

likuwamwezi April, 1960. Nilifika bandarini mwendo wa saa nne asubuhi. Jua lilianza kukolea. Bandarini kulijaa harakati za kila aina. Wachukuzi walikuwa wakienda mbio na marikwama yao yaliyosheheni mizigo. Makuli walikuwa wakipakua na kupakia bidhaa melini. Zogo na kelele, viumbe wakihangaika kutafuta riziki.

M.V. Ubena, meli iliyokuwa ikimilikiwa na kampuni ya Kijerumani ya Deutsch Ost-Afrika Linier, ilikuwa imetia nanga nje ya bandari. Kwa hivyo ilinibidi nipande mashua ili kuifikia pale ilipokuwepo. Wasiwasi ulinijaa na nilihofu asinione mtu aliyenijua akapeleka habari kwetu. Nilitamani ile mashua ipae ili nifike haraka kule melini. Lakini mashua yenyewe iliendeshwa kwa kukoroga kasia moja lililopachikwa kwenye kishwara. Ilikuwa ikijisukumasukuma taratibu ikipigwa na mawimbi yaliyokuwa yakiibuka kutokea kule mbele. Ile mashua ilikuwa mara ipo juu ya mgongo wa wimbi, mara chini ya wimbi, ikipanda na kushuka. Nilijiona kama nisingelifika kule meli ilikotia nanga.

Yule mpiga kasia alikuwa akilikoroga kasia kwa bidii, akibishana na mawimbi na upepo mkali. Mara nyingine maji yalikuwa yakiruka mpaka ndani ya chombo pale mashua ilipopigwa kofi kubwa la wimbi ikayumba huku na huku ukadhani itazama sasa hivi.

Meli ilikuwa mbali. Kwa pale tulipokuwepo, tukititia na kuinuka kwa miinuko na miporomoko ya mawimbi, meli ile ilionekana kama chombo kidogo tu. Kila tulipoikaribia ndipo meli ile ilipodhihirisha ukubwa wake. Hatimaye tulifika na hapo ndipo tulipouona ukubwa hasa wa meli ile. Lilikuwa pandikizi la meli, kubwa utadhani kisiwa. Mimi nilikuwa ndiye abiria pekee mle ndani ya mashua. Nilimlipa mwenye mashua pesa zake nikapanda ngazi tara,tibu kuingia melini.

M.V. Ubena haikuwa meli ya kuchukua abiria. Ilikuwa meli ya kuchukua mizigo. Abiria waliosafiri kwa meli hiyo nao walionekana kama mizigo tu. Melini humo hamkuwa na fursa zozote kwa ajili ya abiria kwa hivyo nilipofika humo melini niliingizwa katika chumba kidogo kilichokuwepo karibu na falka ya nyuma. Chumbani humo mlikuwemo meza moja kubwa. Humo mlikuwa ndimo maskani yangu wakati huo.

Melini humo tulikuwemo abiria wawili. Wa kwanza alikwishaingia melini kabla yangu na mimi nilimkuta humo. Alikuwa mtu wa makamo, alivaa kanzu, kofia ya mkono na kikoi. Kwa ile lahaja yake nilijua kwamba alikuwa mshamba. Nilisalimiana naye nikamwacha vilevile alivyo wala sikutaka kujua yeye ni nani kwa sababu nilijua kwamba tungelikuwa sote kwa safari ndefu ambayo ingelichukua siku nyingi. Kwa sababu hiyo tungelikuwa na muda wa kutosha wa kujuana.

Meli ilikuwa ing'oe nanga jioni kwa safari ya Tanga. Nilikuwa nikiingojea saa ya kuondoka ifike huku nikiwa na wasiwasi tele moyoni. Ilikuwa safari ya utoro kwa hivyo kulikuwa na uwezekano wa wazazi wangu kwenda polisi na kutoa taarifa ya kupotelewa na mtoto wao na polisi kuanza msako. Niliogopa nisionekane na mtu yeyote aliyenijua akapeleka habari kwetu.

Hatimaye meli iling'oa nanga. Ilianza safari taratibu kuelekea kaskazini. Moyo wangu ulitulia. Nikasimama kwenye ukingo wa meli nikiangalia nyuma huku nikiiwacha Zanzibar nyuma yangu. Meli ilipopita Beit-el-ras niliyaangalia majengo ya chuo ambacho kilikuwa ni sehemu ya maisha yangu kwa muda wa kadri ya miaka minne. Hapo ilinijia huzuni ya kuachana na wenzangu nilioishi nao chuoni hapokama ndugu. Pia ilinijia huzuni ya kuachana na baba yangu, mama yangu na ndugu zangu. Nikiachana nao nikiwa sijui ninakokwenda wala sijui nini ungelikuwa mustakabali wangu. Nilikuwa ninakwenda tu, bahati nasibu.

Magharibi yalianza kuingia, Zanzibar nikiiona ileee, ikipotea nyuma yangu taratibu. Mbele yangu ilikuwa imetanda bahari iliyojitandaza mpaka upeo wa macho yangu. Mbinguni kulikuwa kuzuri, kumependeza. Mbingu zilichanua na zilijipanga kwa tabaka ya rangi ya moto mkali. Rangi hiyo ilichanganyika na hudhurungi na zambarau. Jua lilikuwa mdawari mithili ya mpira mkubwa wa moto, lilititia taratibu baharini.

Usiku uliingia, kiza kikatawala. Bahari ilikuwa imetanda pande zote, kimya. Nilikuwa nikiusikia mlio wa meli tu ikinguruma. Meli ikiyumba, mara kulia mara kushoto. Hapo ndipo nilipopata wasaa wa kuzungumza na abiria mwenzangu kwa utulivu.

"Unaitwa nani mwenzangu?" nilimwuliza.

"Ame," alinijibu. Na yeye alionesha hamu ya kutaka kunijua.

"Umetokea wapi na safari ya wapi?" niliendelea kumwuliza.

"Nimetokea Mkokotoni na safari yangu ni mpaka Aden. Nildfika huko nina mpango wa kuendelea mpaka Makka kwenda kuhiji."

"Utafikaje Makka kutoka Aden?" nilimwuliza.

"Magari ya kutoka Aden kwenda Makka yamejaa tele," alinijibu.

Hatukuwa na mengi ya kuzungumza. Tulilala mle ndani ya Idle chumba, mimi nililala juu ya ile meza kubwa na yeye alitandika mkeka aliokuja nao akalala chini. Siku ya pili alfajiri tuliingia Tanga.

Wakati huo sikuwa na wasiwasi tena. Sikuangalia tena nyuma huku nikiwaza labda nitateremshwa melini nirejeshwe nyumbani. Niliangalia mbele tu, Aden, kule nilikotaka kwenda. Niliwaza kwamba ninakwenda Aden, nchi ya ugenini. Nilikuwa simjui mtu, sikuwa na mwenyeji wa kufikia, sikujua ningeishi vipi. Mimi nilikuwa ninakwenda tu. Nilikuwa nina shilingi chache sana mfukoni. Lakini nilikuwa na moyo wa kijasiri. Nilijipa matumaini, nikisema, madhali kuna watu, nitaishi tu.

Tulikaa Tanga kwa muda wa. siku mbili. M.V. Ubena ilikuwa ikibeba mkonge na vinoo vya shaba, usiku na mchana. Ilibeba mkonge na shaba mpaka ikashiba sawasawa, falka zilijaa mpaka juu. Ilichukua na wanyama pori, twiga mmoja na chui mmoja. Walifungwa barabara ndani ya masanduku. Ilibeba na abiria wawili zaidi na sote tukawa abiria wanne. Abiria wale walikuwa Waarabu waliokuwa na asili ya Yemen ambao huku Afrika Mashariki tunawaita Washihri.

Siku ya tatu tuliondoka Tanga kwa safari ya Mombasa.

Kile chumba kidogo tulichokuwa tukilala mimi na Ame nacho kilijazwa mizigo tele. Sote tuliwekwa kwenye deki na hapo palikuwa nd'o maskani yetu kwa muda wote wa safari yetu.

Baada ya safari ya usiku mmoja tulifika Mombasa. Hapo tulikaa kwa muda wa siku mbili meli ikizidi kupakia. Vishilingi vyangu vichache nilivyokuwa navyo nilivimaliza kwa chakula wakati nikiwa Tanga na Mombasa na tulipoondoka Mombasa nilikuwa sina hata senti moja.

Wakati huo sote tulikuwa pale deki tumeanza safari ndefu ya kutoka Mombasa mpaka Aden. Safari ya mwendo wa wiki nzima. Hapo tulizungumza na kujuana zaidi. Wale Waarabu wawili walikuwa wakiishi Tanga lakini mwaka ule, 1960, mapambano ya kupigania uhuru wa Tanganyika yalikuwa yamepamba moto. Kwa mawazo yao walidhani Tanganyika ikipata uhuru yangelizuka machafuko makubwa, kwa hivyo wao waliamua kurudi kwao Yemen mapema. Sote wanne, kila mmoja alikuwa na safari yake. Wale Waarabu wawili walikuwa wanarudi Yemen. Watakapofika Aden wao wangelikuwa wameshafika nyumbani. Ame, yeye safari yake ilikuwa mpaka Makka na mimi mpaka Uingereza.

Nilikuwa sikujiandaa kwa chakula nikiwa safarini. Nilitegemea kuomba chakula mumo humo melini. Siku moja nilipokwenda jikoni kuomba mkate nilimkuta mpishi akitoa jichwa la nguruwe kutoka kwenye oven. Nilisema moyoni mwangu "Mama yangu we!" Mimi Muislamu, sili nguruwe na inaonesha nguruwe nd'o kilichokuwa chakula chenyewe melini mle." Nilisema, "Potelea mbali, msafiri kafiri, hata huyo nguruwe nikimpata nitamla."

Ame, alichukua pakacha moja la machungwa na pakacha moja la muhogo. Mategemeo yake yalikuwa kwamba atakapofika Aden angeliyauza hayo machungwa na huo muhogo ili apate pesa ambazo zingelimsaidia kwa safari yake yaMakka. 

Wale Waarabu wawili, wao walijiandaa vizuri kwa safari yao. Wao ndio waliotuafu tusiadhirike kwa njaa ndani ya meli ile. Walichukua mchele wa kutosha, mafuta ya kupikia, nyanya za makopo, vinengwe kwa wingi na viungo tele. Walikuwa na jiko la stimu na vyombo kamili vya kupika.

Safari ilikuwa imeshtadi. Tulikuwa katikati ya bahari kuu hatuoni chochote isipokuwa bahari kusini, bahari kaskazini, bahari mashariki, bahari magharibi. Chombo kilinguruma na kuyumba huku na huku. Mawimbi yakipanda na kushuka. Tulizihesabu siku moja moja. Ilipofika usiku, mawazo ya nyumbani yalinijia nikawawaza baba, mama na ndugu zangu. Nilijua kuwa walipata tabu kunitafuta. Nilijua kwamba roho zao zilikuwa juu juu, hawakuwa na raha. Mchana, wakati mwingi nilikuwa nikisimama kwenye ukingo wa meli na kuangalia baharini. Lakini hapo palikuwa hakuna chochote cha kuangalia isipokuwa bahari yenyewe. Labda na wale samaki wadogo waliokuwa wakiruka kama panzi.

Hatukuwa na mengi ya kuzungumza na abiria wenzangu.

Wale wawili kila wakati waliongea kwa Kiarabu kwa hivyo hawakuwa na muda wa kuongea na sisi. Ame yeye akili yake yote ilikuwa Makka. Mara moja moja alinihadithia utukufu wa mji huo na fahari ambayo angeliiona kwa kufika huko, katika mji huo mtakatifu. Alikuwa akiomba afie huko huko kwani aliamini kwamba anayefia Makka wakati wa Hijja basi huyo ni mja wa peponi bila ya hesabu.

Humo melini tuliishi kwa kufadhiliwa na wale Waarabu.

Chochote kile walichokipika, tulikula sote. Mara moja moja nilikuwa nikenda jikoni na wapishi walikuwa wakinigawia makombo ya mikate waliyoisaza. Machungwa ya Ame yalianza kuoza na mihogo ilianza kuvunda hata kabla hatukufika nusu ya safari yetu. Machungwa tuliyala mojamoja na yaliyoharibika Ame aliyatosa baharini. Mihogo tuliitafuna hivyohivyo mibichi. Ile iliyoharibika nayo Ame aliitosa baharini. Kwa hivyo zile bidhaa ambazo Ame alizichukua akitegemea kwamba angeliziuza atakapofika Aden ili zimpatie pesa kidogo, ziliishia ama kuliwa au kutoswa baharini.

Kila tulipozidi kuelekea kaskazini ndivyo bahari ilivyozidi kuwa chafu. Tulikuwa tukielekea kwenye pembe ya Afrika, kule iliko Ras Gardafui. Wakati mwingine meli ilikwenda mrama ukadhani sasa hivi ingelizama. M.V. Ubena, na ukubwa wake wote, ilikuwa kama kinyangarika tukilichokuwa kikiyumbishwa huku na huku. Mara nyingine, wakati ilipolala upande mmoja, tulidhani isingelikaa sawa tena. Wakati mwingine sote tulilewa bahari tukakaa pale kwenye deki tukidorora tumeshikwa na mkunguru. Juu ya zahama zote hizo na vishindo vya bahari iliyokuwa ikivurumisha mawimbi makubwa makubwa, M.V. Ubena ilikuwa ikisonga mbele. Ilikuwa imara, ikinguruma tu huku ikiyakata mawimbi moja baada ya jingine.

Hatimaye tulianza kuyaona majabali kwa mbali. Yalikuwa yamesimama mbele yetu kama vichuguu vya mchwa vilivyojipanga kule kwenye upeo wa macho yetu. Tulijua kwamba tukikaribia Bara Arabu na Aden haikuwa mbali na sisi.

Siku ya pili alfajiri M.V. Ubena ilipiga sero kutoa ishara ya kuwa ilikuwa milangoni mwa bandari ya Aden. Ilikuwa inataka kuingia ndani. Haikuchukua muda, mataboti ya rubani ilifika pembezoni mwa meli. Rubani alishushiwa ngazi na kuingia melini. Aliipitisha meli katika mlango wa bandari ya Aden. Kiasi cha saa nne asubuhi meli ilitia nanga. Mji wa Aden ulikuwa mbele yetu umesimama chini ya majabali makubwa makubwa.

Harakati za watu waliokuwa wakipanda melini zilianza. Maafisa wa uhamiaji, maafisa wa afya na wakala wa ile meli walikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuingia ndani ya meli. Siku ile nilikoga nikatakata. Nilivalia vizuri ili nionekane mtanashati nitakapoingia mjini Aden. Niliona kama nusu ya ndoto yangu ilikuwa kweli na ngwe ya kwanza ya safari yangu niliimaliza kwa mafaniko.

Abiria  sote  wanne tulikuwa tumesimama sanjari. Tulikuwa tukisubiri kuingia ndani ya chumba ambacho Afisa wa Uhamiaji aliweka ofisi yake ya muda ndani ya meli ile. Mimi nilikuwa nimesimama na mfuko wangu mkononi. Hamu ilikuwa imenijaa moyoni. Lakini hamu yenyewe ilikuwa imechanganyika na wasiwasi kwani pale Aden nilikuwa simjui mtu yeyote. Ilikuwa nishuke pale bahati nasibu tu. Sik Jua ningeliishi wapi. Sikujua ningeishi vipi. Sikujua ningelikula nini. Yote hayo nilimwachia Mungu nikiamini ndani ya moyo wangu kwamba Mungu hamnyimi mja wake riziki.

Tulikuwa tumejipanga, tukiingia mmoja mmoja ndani ya chumba cha Afisa wa Uhamiaji. Aliingia yule Mwarabu wa kwanza. Aligongewa muhuri akatoka. Aliingia Mwarabu wa pili. Naye aligongewa muhuri akatoka. Niliingia mimi. Nilitoa pasi yangu ya kusafiria nikaiweka juu ya meza ya yule Afisa wa Uhamiaji. Alikaa juu ya kiti nyuma ya meza kubwa. Alikuwa amevaa sare ya kotijeupe na suruali kipande nyeupe. Alikuwa mnene kama pipa. Kinywani alikuwa amejaa meno ya dhahabu jasho likimtoka na kujifuta kwa kitambaa.

Aliifungua pasi yangu ya kusafiria na aliipekua ukurasa mmoja baada ya mwingine. Ilikuwa bado mpya, haikutumika hata mara moja. Alifungua ukurasa uliokuwa na picha yangu ili kuhakikisha kama ni mimi hasa ndiye niliyekuwa mwenye pasi ile ya kusafiria. Picha ilikuwa ni yangu hasa na mimi nilikuwa nikimtazama yeye kwa macho yangu ya kitoto.

"Wewe mwanafunzi?"  Aliniuliza kwa lugha ya Kiingereza.

"Ndiyo," nilimjibu.

Alijifuta jasho kwa kitambaa akanitazama na kuniuliza tena, "Umekuja kufanya nini Aden?"

"Napita kwa muda tu halafu naelekea Uingereza," nilimjibu.

"Unazo shilingi mia sita?" aliniuliza.

"Sina," nilimjibu.

"Huwezi kushuka Aden mpaka uweke dhamana ya shilingi mia sita," aliniambia huku akiwa amenikazia macho, akinitazama.

Sikujua kwa nini nilitakiwa nilipe dhamana ya shilingi mia sita kwa sababu Aden wakati huo ilikuwa ni koloni ya Mwingereza. Mimi pia nilikuwa na pasi ya kusafiria ya Kiingereza. Alichotakiwa kufanya yule Afisa wa uhamiaji ilikuwa ni kunigongea muhuri tu wa kuniruhusu kuingia

nchini bila ya masharti yoyote yale.

« Tafadhali nakuomba uniruhusu niingie nchini na hapo nitakapozipata nitakuleteeni ofisini kwenu," nilimwomba kwa unyenyekevu.

"Hapana," alinijibu kwa ufupi. Bila ya kunieleza chochote zaidi, aligonga muhuri ndani ya pasi yangu ya kusafiria halafu aliuchora ule muhuri alama ya kujumlisha kwa kalamu yake ya rangi nyekundu.

Nilihisi sasa nimegonga mwamba. Kilichobaki ilikuwa ni kurejeshwa Zanzibar nikaanze alifu kwa ujiti. "Haiwezekani," nilisema moyoni mwangu.

Kile chumba kilikuwa kimezidi watu. Nahodha wa M.V. Ubena alikuwa pale, wakala wa kampuni ya meli alilrnwa pale, maafisa wengine wa uhamiaji walikuwa pale. Wote walikuwa wamenizunguka mimi.

Nilimwomba yule wakala, "Tafadhali nilipie shilingi mia sita nitakurudishia nitakapozipata nikiruhusiwa kushuka." 

Wasifu wa yule wakala ulionekana kama ni Msomali tena alikuwa na sura ya mtu mwenye huruma. Lakini kinyume na nilivyofikiria, alinikatalia ombi langu katakata. Sidhani kwamba kunikatalia kwake kulikuwa ni kwa ajili ya utovu wa huruma. Alikuwa lazima akubaliane na kanuni na sheria za nchi ile.

Nilimgeukia nahodha wa ile meli. Nilimwomba nakumsihi aniruhusu nibakie ndani ya meli yakee kama mfanyakazi, hata bila ya malipo, mpaka mwisho wa safari ya meli hiyo. Naye alinikatalia. Ikawa ni kurudishwa Zanzibar, tena haraka kaina ilivyowezekana.

Kazi ilikuwa pale ilipofika zamu ya mwenzangu, Ame, kuhojiwa na yule Afisa wa Uhamiaji. Ame alikuwa hajui Kiingereza naye Afisa Uhamiaji hajui Kiswahili. Ulizuka mtafaruku, wote hawakuelewana. Kelele alizozipiga Ame,vurugu aliyoifanya, yote hayo hayakumsaidia kitu chochote. Hatima yake ilikuwa kama yangu nayo ni kurudishwa Zanzibar.

Nilivunjika moyo, nilikata tamaa, nikaona jitihada yangu yote niliyoifanya sikupata matilaba yangu, narudishwa kule kule nilikotokea. Mimi na Ame tulishushwa melini tukaingia ndani ya mashua pamoja na wakala wa ile me.li Sote tulikuwa wahamiaji wasiotakiwa ndani ya nchi ile. Mwenye mashua alipiga makasia na taratibu tulielekea kwenye bandari ya Aden.

Hapo ndipo nilipoyaona majabali ya mji ule ambayo kule mbali tulipokuwa baharini tukiikaribia bandari niliyaona kama vichuguu tu. Yalikuwa majabali makubwa makubwa yaliyosimama nyuma ya ule mji. Utadhani yangeliporomoka yakisagesage kila kitu kilichokuwa chini yake. Lakini hayakuporomoka. Yalikuwapo tu, yamesimama vilevile. Joto kali lilikuwa likifukuta, jua likiwaka kama moto. Tuliposhuka mashuani, gari la wakala lilikuwa likitusubiri. Tuliingia humo na tulipelekwa moja kwa moja mpaka kwenye ofisi ya wakala huyo.

Hapo  ofisini  pake  nilizidi  kumsihi  na kumwomba anisaidie lakini hata hakunisildliza. Alikuwa ameshughulika akipiga simu kutafuta chombo chochote kile kilichokuwa kikielekea· Zanzibar, tupakiwe ndani ya chombo hicho, tuondoke Aden. Hatukutakiwa kuonekana ndani ya nchi ile. Mimi na Ame tulibakia kutazamana tu. Hatukuwa na la kufanya. Ndoto zetu ziliyeyuka. Matumaini yetu yalivurugika. Tulikata tamaa, tulivunjika moyo. Pale nilipokuwa nimekaa nilikuwa nikiwaza. Kurudi tena Zanzibar, chuoni nimetoroka, nyumbani nimetoroka, wenzangu nilikwishawaaga na kuwambia kwamba ile ilikuwa ni safari ya Ulaya tu. Hapana kurudi nyuma. Nilihisi kurudi Unguja ni kurudi na tahayuri na wingi wa fedheha. Ningeliwatazamaje wenzangu? Nilikaa pale nikiwaza. Kumbe mbio zangu zote zile zilikuwa ni mbio za sakafuni tu na sasa zimeishia ukingoni. Ni kurudi kulekule nilikozianzia. Nilitamani kumtoroka yule wakala, nikimbie niingie ndani ya mitaa ya Aden asinione tena. Lakini ningelikwenda wapi katika mji ule uliozungukwa na majabali kila pembe. Sikuwa ila niliyemjua, sikuwa na nilipopajua.

Kwa bahati tu, mle ofisini mwa yule wakala nilimwona mtu niliyemjua. Sijui kama na yeye akinijua wala sikujua ni shughuli gani iliyompeleka pale kwa yule wakala. Alikuwa daktari mashuhuri wa meno nchini Zanzibar. Nilimjua kwa zile ziara zake za mara kwa mara katika skuli yetu ya Gulioni. Alikuwa akija kukagua na kuwatibu wanafunzi waliokuwa na maradhi ya meno. Akiitwa Dokta Idarusi Baalawi. Nilidhani angeliweza kunisaidia ili nitoke katika msukosuko uliokuwa umenikabili. Lakini hata baada ya kumwomba msaada hakuweza kunisaidia. Nadhani hata angelitaka kunisaidia asingeliweza kufanya hivyo kwa sababu nilikwishakabidhiwa kwa wakala wa meli na maafisa wa uhamiaji. Maagizo aliyopewa yule wakala yalikuwa ni kunirudisha nilikotoka tu, basi. Yule wakala ilimlazimu atekeleze wajibu wake.

Used by permission of Longhorn Publishers PLC.